Mjumbe wa UN Achunguza Mauaji Kenya

  • Mwai Gikonyo

Mjumbe huyo wa Umoja wa Mataifa, Profesa Phillip Alston anayechunguza mauaji yaliyofuatia uchaguzi mkuu nchini Kenya, amepata ushahidi kutoka kwa watu ambao ndugu zao waliuawa katika ghasia hizo, na kutembelea kanisa ambapo wanawake na watoto kadhaa waliteketezwa kwa moto wakiwa hai.

Profesa Alston amefanya mashauriano na maofisa wakuu wa serikali na polisi, na kutembelea eneo la magharibi ambapo watu kadhaa waliuawa, kujeruhiwa na mamia wengine kulazimika kuyakimbia makazi yao.

Akiwa Rift Valley katika jimbo la Eldoret, Alston anasema amefanikiwa kupata ushahidi kutoka kwa watu waliopoteza ndugu zao, na kwamba katika mazungumzo yake ya faragha, ameweza kupata ushahidi wa watu wanaodai kuwa ndugu zao waliuawa na maofisa wa jeshi na polisi.

Licha ya kwamba jeshi la Kenya limekuwa likikanusha kuhusika na mauaji hayo, wanawake kadhaa, wengi wao kutoka mlima Elgon, wamejitokeza na kusema waume zao walichukuliwa na kuuawa na maofisa wa jeshi na polisi.