Mjadala unaendelea nchini Kenya kuhusu hatma ya watuhumiwa wa machafuko na maafa yaliyofuatia uchaguzi mkuu wa nchi hiyo uliofanyika Disemba 2007, huku baadhi wakitaka watuhumiwa washitakiwe katika mahakama maalum ya nchi hiyo, na wengine wakitaka wapelekwe katika mahakama ya kimataifa,The Hague.
Hassan Omar, makamu rais wa tume ya kitaifa haki za binadamu nchini Kenya, anasema tume yake ingependa watuhumiwa washitakiwe katika mahakama maalum ya nchi hiyo, hali ambayo anasema itasaidia kuwafanya wananchi wawe na imani na taasisi zao wenyewe.
Omar anasema mahakama maalum itaweza kufanya kazi yake kwa urahisi na ufanisi zaidi kwa sababu kesi zitakuwa zikiendeshwa nchini hapo ambapo mauaji hayo yalitendeka, na itakuwa rahisi kupata mashahidi katika kesi hizo.