Zaidi ya 111 Wauwawa kwa Moto Kenya

Watu wapatao 111 wamekufa kwa moto nchini Kenya na zaidi ya 200 kujeruhiwa baada ya lori lililokuwa limebeba mafuta kupinduka kwenye njia kuu kati ya miji ya Nakuru na Eldoret. Mamia ya watu walikuwa wamekusanyika kuzoa mafuta yaliyokuwa yakivuja, wakati gari hilo liliporipuka Jumamosi na kuwaka moto.

Shirika la Msalaba Mwekundu nchini Kenya linasema maofisa wa polisi waliofika eneo la tukio, wanawake na watoto ni miongoni mwa waathirika wa moto huo. Bado chanzo cha moto huo hakijajulikana, lakini baadhi ya ripoti zinasema sigara iliyodondoshwa chini huenda ndio chanzo cha moto huo.

Waziri Mkuu Laira Odinga na mawaziri kadhaa walifika eneo la tukio Jumapili. Bwana Odinga alielezea kusikitishwa kwake na watu walioathiriwa na moto huo, lakini pia akaonya kuhusu hatari ya kukusanya mafuta yanayovuja na kukumbusha kuwa ajali kama hizo zimewahi kutokea nchini Kenya.