Waislamu Kenya Wataka Guantanamo Bay Ifungwe

Viongozi wa kiislamu nchini Kenya wameunga mkono hatua ya Rais Barack Obama wa Marekani kusitisha kesi zinazowakabili washukiwa wa ugaidi na kumtaka afunge gereza la Guantanamo Bay, ambalo wanadai kuwa linatumika kukiuka haki za binadamu.

Viongozi hao wamesema kuwa gereza hilo limekuwa likitumika kukandamiza waislamu na kwamba kufungwa kwake kutasaidia kuboresha uhusiano kati ya Marekani na mataifa ya kiislamu.

Sheikh sheikh Jumangao wa Baraza Kuu la Waislamu nchini Kenya amesema, "Msimamo wetu ni kwamba, jela ya Guantanamo Bay ni lazima ifungwe," na kuongeza kuwa tayari kunadalili kuwa Rais Obama ameanza kutekeleza baadhi ya ahadi alizotoa wakati wa kampeni za uchaguzi.

Kabla ya sherehe za kuapishwa bwana Obama kufanyika Jumanne, kulikuwa na mvutano nchini Kenya kuhusu kuwakilishwa kwa serikali ya nchi hiyo katika sherehe hizo. Baadhi ya viongozi wa Kenya walidai kuwa wangehudhuria sherehe hizo, lakini ubalozi wa Marekani nchini humo ulisema kuwa hakuna mwaliko uliokuwa umetolewa.