Zanzibar Yaadhimisha Miaka 45 ya Mapinduzi

Wananchi wa Zanzibar wameadhimisha miaka 45 ya mapinduzi huku rais Abeid Amani Karume akitoa wito kwa chama cha upinzani CUF kufungua ukurasa mpya kwa kurejea kwenye meza ya mazungumzo kuupatia ufumbuzi mzozo wa kisiasa wa Zanzibar.

Rais Karume ametoa wito huo wakati wa kilele cha sherehe za mapinduzi zilizofanyika kwa mara ya kwanza kisiwani Pemba tangu alipoingia madarakani mwaka 2000.

Katika hotuba yake Bwana Karume amesema mashauriano kati ya chama tawala CCM na CUF yaliendelea kupitia kamati ya pamoja ya vyama hivyo, na kwamba sehemu kubwa ya ajenda za mazungumzo ilikubaliwa na pande zote mbili, na kwamba ni sehemu ndogo tu ambayo haikufikiwa.

Amesema kutokana na hali hiyo, jambo la msingi kwa sasa ni kuendelea na utamaduni wa kuzungumza kwa uwazi zaidi kupitia vikao rasmi, ili kupata ufumbuzi wa tofauti zilizo jitokeza.

Laki baadhi ya wananchi wa visiwa vya Pemba na Unguja wanasema hawaoni mabadiliko yoyote tangu yalipo fanyika mapinduzi visiwani humo miaka 45 iliyopita.