Ndege za Israel zimeshambulia tena leo vituo mbalimbali zikiwemo wizara za serikali na jengo la bunge la kimkoa huko Gaza, kituo cha polisi katika eneo la Rafah kusini mwa Gaza, na njia za chini kwa chini kwenye mpaka wa Israel na Gaza.
Duru za kiusalama za Hamas zimesema kiongozi wa kisiasa, Nizar Rayyan aliuwawa wakati wa shambulio hilo pamoja na familia yake. Rayyan alikuwa mwanaharakati aliyetaka kuanzishwa upya kwa mashambulio ya kujitoa mhanga dhidi ya taifa hilo la kiyahudi.
Mwandishi wa habari wa Palestina aliyepo Gaza, Mohamed Dawwa, ameiambia Sauti ya Amerika kwa njia ya simu kuwa mashambulio ya Israel yameendelea usiku mzima.
Dawwa anasema, "Hatukuweza kulala tangu wakati huo. Inazorota sana. Hali kwangu mimi, ilikuwa ni usiku mbaya kabisa, hii leo ilitarajiwa kuanza mwaka mpya. Na hadi hivi leo mabomu yanaendelea kusikika pamoja na mizinga, na nimeshuhudia mimi mwenyewe."
Israel inasema inalenga wanaharakati wenye ushirikiano na mashambulio ya roketi na miundombinu ya Hamas, kundi la kiislamu linalodhibiti Ukanda wa Gaza.