Ndege za jeshi la Israel zimeendelea kushambulia vituo vya Hamas Jumanne Ukanda wa Gaza huku kundi la wanamgambo wa Hamas likiahidi kurusha roketi ndani zaidi ya taifa hilo la Kiyahudi kuliko ilivyowahi kutokea.
Watu kumi wanaripotiwa kuuwawa katika mashambulio hayo ya ndege za Israel ambazo zimeteketeza majengo ya serikali ya Hamas na jengo moja linalo milikiwa na chuo kikuu cha kiislam.
Wanajeshi wa Israel, vifaru na magari mengine ya kijeshi wamejipanga kwenye mpaka wa Israel na Gaza tayari kwa mashambulio ya nchi kavu.
Wakati hayo yakiendelea, rais Hosni Mubarak wa Misri amelaani oparesheni za jeshi la Israel Ukanda wa Gaza na kuzitaka pande husika, Israel na wanamgambo wa Hamas kuendelea na usitishwaji mapigano.
Katika hotuba yake iliyotangazwa na kituo cha televisheni ya taifa, bwana Mubarak ameiomba Israel kusitisha mara moja oparesheni zake za kijeshi Gaza.