Raila: Lazima Mugabe aondolewe

Ingawa Rais Robert Mugabe wa Zimbawe alitangaza mwishoni mwa wiki kwamba serekali yake imefanikiwa kuzuia ugonjwa wa kipindupindu, lakini watu wengi wanazidi kufuariki kutokana na ugonjwa huo kufuatana na takwimu za Umoja wa Mataifa.

Akihudhuria mazishi ya afisa mmoja wa chama tawala siku ya Alhamisi, Rais Mugabe alirudia tena tuhuma kwamba nchi za Magharibi zinataka kutumia tatizo la kipindupindu kama kisababu cha kuipindua serekali yake.

Alisema "kwa sababu ya kipindupindu, Bw Brown anataka hatua ya kijeshi ichukuliwe. Sarkozy anataka hatua ya kijeshi. Bush anataka hatua ya kijeshi, kwa sababu ya kipindupindu. Lakini mimi ninafuraha kusema, madaktari wetu wakisaidiwa na wengine na Shirika la Afya Duniani WHO wamezuia kipindupindu. Kwav hivyo hakuna haja tena ya vita"

Akizungumza na Sauti ya Amerika waziri mkuu wa Kenya Bw Raila Odinga amesema "changamoto kubwa wa Umoja wa Afrika ni kuonesha wanauwezo wa kusikiliza mwito wa watu wa Afrika. Kwa sababu AU imepewa jukumu la kuona kwamba demokrasia inadumishwa katika bara la Afrika"

Bw Raila anasema kunahaja ya kuchukuliwa hatua za haraka kuiwekea Zimbabwe vikwazo kamili vya kiuchumi ili kuhakikisha utawala wa Mugabe unaangushwa na kuokoa maisha ya wananchi wa Zimbabwe.