Magaidi Washambulia India

  • Abdushakur Aboud

Baada ya kufanya kazi ya kuwaondoa watu katika hoteli mbili za kifahari zilizoshambuliwa na magaidi mjini Mumbai, makamanda wamezindua leo oparesheni katika maeneo matatu yaliyozingirwa na washambuliaji hao zikiwemo hoteli hizo mbili.

Raia kadhaa wa kigeni bado wanaendelea kushikiliwa mateka na magaidi katika hoteli ya Oberoi, na maafisa wanasema miongoni mwa watu zaidi ya 100 waliouwawa ni raia mmoja wa Uingereza, raia wa Japan na mwingine kutoka Australia.

Akihutubia taifa, waziri mkuu wa India Manmohan Singh amesema washambuliaji walichagua maeneo yanayovutia wageni ili kuzusha hali ya taharuki na kuleta wasiwasi katika mji mkuu wa biashara.

Bwana Singh ameahidi kuwa serikali yake itachukua hatua mathubuti kuhakikisha mashambulizi kama hayo ya kigaidi hayatokei tena. Ameonya mataifa jirani ambayo anasema yanahifadhi magaidi kuwa itawagharimu kama hawatachukua hatua muafaka dhidi ya magaidi hao.