Miezi kumi na moja tangu machafuko ya baada ya uchaguzi kutokea nchini Kenya, wakimbizi wa ndani kwa ndani wanaendelea kusononeka katika kambi wanapoishi, licha ya serikali ya nchi hiyo kusema mpango wa kuwarejesha makwao umepata ufanisi mkubwa.
Wiki chache zilizopita akina mama wakimbizi walikusanyika nje ya majengo ya bunge jijini Nairobi wakitaka wabunge wasikie kilio chao, badala yake walitimuliwa kwa kupigwa gesi ya kutoa machozi.
Akizungumza na Sauti ya Amerika kutoka mji wa Eldoret, Meja mstaafu John Seii ambaye ni mwenyekiti wa shirika la North Rift lisilokuwa la Kiserikali, alisema wakimbizi bado wanateseka katika kambi.
Meja Seii alisema wengi wa wakimbizi hao wanakabiliwa na matatizo ya afya na hawajui ni lini watarejeshwa makwao kuanza ujenzi mpya wa maisha yao, hali ambayo inawafanya kukosa matumaini ya maisha yao ya baadaye.