Rais mteule wa Marekani Barack Obama amewatangaza leo Jumatatu maofisa wa juu wanaounda timu yake ya kiuchumi, akiwemo Timothy Geithner rais wa benki ya kitaifa mjini New York ambaye atakuwa waziri wa fedha.
Bwana Obama amesema ni muhimu kuweka tayari timu yake ya wanauchumi mapema ili kuanza kulitafutia ufumbuzi tatizo la uchumi wa Marekani ambapo uuzaji wa hisa umeporomoka zaidi katika kipindi cha miaka mitano, watengenezaji magari wakiwa hatarini kufunga viwanda vyao, na mamilioni ya wamarekani wakiwa hatarini kupoteza ajira na nyumba zao.
Amesema, "Tunakabiliwa na tatizo kubwa la kiuchumi kuwahi kutokea katika historia yetu--masoko yetu ya kifedha yamedidimia--na ununuzi wa nyumba umepungua sana mwezi Octoba kuwahi kutokea katika kipindi cha miaka 50 iliyopita."
Rais wa benki ya akiba ya kitaifa mjini New York Timothy Geithner amechaguliwa kuongoza wizara ya fedha ya Marekani. Geithner anauzoefu katika sekta mbalimbali za mabenki ya Marekani, na rais mteule anatumaini kuwa chaguo lake hilo litapeleka ujumbe kuwa utawala unaoingia madarakani unaelewa fika matatizo sugu yanayo kabili uchumi wa Marekani.