Wakazi mashariki mwa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo wemekaribisha ziara ya mwishoni mwa wiki ya mjumbe maalum wa umoja wa mataifa, ambaye pia ni rais wa zamani wa Nigeria Olusegun Obasanjo, wakielezea matumaini yao kuwa mazungumzo baina yake na rais Joseph Kabila, na pia kiongozi wa waasi wa nchi hiyo Jenerali Laurent Nkunda yatazaa matunda.
Akizungumza na Sauti ya Amerika, Profesa Gervas Chiralirwa, mtetezi wa haki za kiraia nchini DRC amesema wakazi wa eneo la mashariki lililokumbwa na vita wanaendelea kutaabika kwa kukabiliwa na changamoto za kimaumbile, ikiwemo mvua kubwa na baridi kali baada ya kulazimika kuondoka majumbani mwao.
Profesa Chiralirwa amesema wakazi hao wanataka rais Kabila na Jenerali Nkunda waache kiburi chao na kuzungumza ana kwa ana kwa maslahi ya wananchi. Ameeleza masikitiko yake kuwa kina mama na watoto wanalala njaa na hawana matumaini na hali ya baadaye.