Viongozi wa G-20 wakutana Washington

Viongozi wa kundi linalojulikana kama G-20, linalochanganyisha mataifa tajiri ya viwanda na yale yanayoinukia kiviwanda wanakutana mjini Washington kujadili hatua za kudumisha utulivu wa mzozo wa fedha duniani. Viongozi wa nchi za Ulaya waliongoza juhudi hizi za kuwepo na mkutano utakaoleta suluhisho kwa mzozo wa kiuchumi unaokumba dunia nzima.

Umoja wa ulaya ulitangaza siku ya ijumaa kwamba uchumi wa mataifa yote 13 yanayotumia sarafu ya Euro umedumaa. Na wakati mzozo wa uchumi wa Ulaya ulipoanza kujitokeza viongozi wawili wenye ushawishi mkubwa Rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy na waziri mkuu wa Uingereza Gordon Brown, walijitokeza kwanza kuongoza juhudi za kupunguza athari za mzozo huo.

Mkutano wa Washington utazingatia kuchukua hatua kama, marekebisho ya masharti na kanuni za kifedha katika lengo la kurudisha ustawi wa uchumi duniani. Na viongozi hao watajadili wakizingatia utawala wa Marekani utabadilika hapo mwakani. Viongozi wa Ulaya wanamatumaini kwamba rais mteule wa Marekani Barack Obama ataweza kurudisha tena nguvu za kiuchumi za Marekani na hapo kuweza kusaidia uchumi wa Ulaya kurudi ulivyokua.