MIAKA 10 YA SHAMBULIZI LA MABOMU BALOZI ZA MAREKANI – KENYA NA TANZANIA.

August 7, 2008 ilikuwa siku iliyokamilisha miaka 10 tangu mashambulizi ya mabomu yaliyotokea kwa wakati mmoja katika balozi za Marekani mjini Nairobi, Kenya na Dar es Salaam, Tanzania. Maadhamisho ya miaka hiyo 10 yalifanyika Nairobi na Dar es Salaam. Watu 218 waliuawa Nairobi, na wengine elfu tano kujeruhiwa wakati huko Dar es Salaam watu 11 waliuawa na wengine 85 kujeruhiwa.

Mamia ya watu walijazana katika ukumbi wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani hapa Washington, na maelfu katika balozi za Marekani huko Nairobi na Dar es Salaam kuadhimisha siku hiyo. Mashambulizi hayo ya malori yaliyojazwa mabomu yaliharibu majengo ya balozi zote mbili, lakini uharibifu zaidi ulikuwa katika ubalozi wa Marekani Nairobi ambako sehemu ya jengo hilo na majengo kadha ya jirani yaliharibiwa vibaya.

Maadhimisho hayo yalifanya huku polisi wa Kenya wakiwa wanafanya msako mkali dhidi ya mtuhumiwa mkuu wa mashambulizi hayo, Fazul Abdullah Mohammed – mzaliwa wa Comoro – ambaye inasemekana aliongoza matayarisho na utekelezaji wa mashambulizi hayo.

Waathirika wa mashambulizi hayo kote nchini Kenya na Tanzania wangali wanalalamika kuwa serikali za nchi hizo pamoja na Marekani hazijawashughulikia ipasavyo kutokana na mkasa huo. Hata hivyo, ubalozi wa Marekani huko Tanzania ulitoa taarifa kusema kuwa waathirika wote walipata fidia za namna fulani na mipango inaendelea, ikiwa ni pamoja na mipango ya elimu kwa watoto wa waathirika.