Nigeria na India zaimarisha ushirikiano wa usalama

  • VOA Swahili

Waziri mkuu wa India Narendra Modi (kushoto) akishika hati ya medali kuu ya heshima ya Nigeria Grand Commander of the Order of the Niger (GCON) aliyokabidhiwa na rais Bola Tinubu(kushoto) hapo Novemba 17, 2024.

Nigeria na India zimekubaliana Jumapili, kuimarisha ushirikiano wao katika usalama wa usafiri baharini, masuala ya ujasusi, na vita dhidi ya ugaidi wakati wa ziara ya kitaifa ya waziri mkuu wa India Narenda Modi.

Modi amekutana na Rais Bola Tinubu na kurudia tena kile wanachokieleza ni kuimarisha ushirikiano wa usalama kati ya mataifa yao makuu ya Asia na Afrika.

Taarifa iliyotolewa na ikulu ya Abuja, inaeleza kwamba viongozi hao wawili walijadili juu ya masuala ya kiuchumi, ulinzi, huduma za afya na usalama wa chakula kati ya nchi zao.

Waziri mkuu wa India alikua Abuja siku ya Jumapili kituo chake cha kwanza katika safari kuelekea kwenye mkutano wa mataifa tajiri dunaini wa kundi la G20 nchini Brazil na baadae Guyana.

Waziri mkuu wa India Narendra Modi (kushoto) akikaribishwa katika ikulu ya Abuja na rais wa Nigeria Bola Tinubu (kulia) Novemba 17, 2024.

New Delhi imeeleza ziara hiyo kama ni mkutano kati ya viongozi wa taifa kuu la kidemokrasia duniani na taifa lenye wakazi wengi barani Afrika, na ni ushirikiano wa kawaida kwani mataifa haya mawili yanajaribu kupigania jukumu kubwa zaidi katika masuala ya kimataifa.

Akizungumza kabla ya mazungumzo yao, Modi amesema, ushirikiano wao uko imara na kuna nafasi nyingi mpya za kuimarisha uhusiano huo.

Ziara inafanyika wakati kumekua na shinikizo jipya kutoka Nigeria na India la kupewa kiti cha kudumu kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.