NATO inafahamu Ukraine ina mahitaji ya dharura dhidi ya Russia; anasema Rutte

Katibu Mkuu mpya wa NATO, Mark Rutte akizungumza na waandishi mjini Brussels. October 1, 2024.

Katibu Mkuu mpya wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO Mark Rutte, amesema leo Alhamis kuwa muungano huo unafahamu Ukraine ina mahitaji ya dharura katika mapambano yake dhidi ya uvamizi wa Russia, wakati alipoitembelea Kyiv kwa mazungumzo na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy.

Rutte aliwaambia waandishi wa habari kuwa ni muhimu kwake kwenda Ukraine wakati huu ili kuelezea wazi, kwa watu wa Ukraine na kwa kila mtu anayeangalia kwamba NATO inasimama na Ukraine. Rutte alisema yeye na Zelenskyy walizungumzia maeneo ambayo Ukraine inahitaji msaada wa ziada, na njia ambazo washirika wa NATO wanafanya kazi ili kukidhi mahitaji hayo.

NATO inasimama na Ukraine, kwa usalama wako na usalama wetu, alisema. Zelenskyy amesema alizungumzia “mpango wake wa ushindi” na kusisitiza wito kwa washirika wa Ukraine kutoa silaha ili kuruhusu silaha hizo kutumika kushambulia maeneo ndani ya Russia.