Waziri wa mambo ya nje wa Marekani azuru Cairo katika juhudi za kusitisha mapigano Gaza

Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri Badr Abdelatty (Kulia) akionyesha ishara anapoondoka na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken baada ya mkutano wao wa pamoja na waandishi wa habari kwenye Ikulu ya Tahrir katikati mwa Cairo Septemba 18, 2024.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken anatumai kusukuma mbele  juhudi za kufanikisha sitisho la vita huko Gaza na kuimarisha uhusiano na Misri anapozuru Cairo Jumatano, msemaji wake alisema, huku kukiwa na wasiwasi kuhusu kuongezeka kwa mivutano huko Mashariki ya Kati.

Ziara ya mwanadiplomasia huyo wa juu wa Marekani inakuja wakati eneo hilo likiwa katika hali ya tahadhari kubwa kutokana na hatari ya vita vya Gaza kupanuka, hasa baada ya kundi la wanamgambo wa Hezbollah kuahidi kulipiza kisasi dhidi ya Israel, likiishutumu kwa kutegua vifaa vya mawasiliano nchini Lebanon siku ya Jumanne.

Israel imekataa kujibu maswali kuhusu milipuko hiyo. Takriban watu tisa walikufa na wengine karibu 3,000 walijeruhiwa.

Akizungumza katika kikao cha kawaida, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje Matthew Miller alisema ni mapema mno kusema iwapo tukio la Lebanon litaathiri mazungumzo ya kusitisha mapigano Gaza lakini amesema Marekani inaamini kuwa diplomasia ndiyo njia ya kupunguza mivutano.