Jeshi la Ukraine, Jumatano liliharibu ndege zisizo na rubani 19 kati ya 20 zilizorushwa na Russia, katika mashambulizi ya usiku kucha, lakini maafisa wamesema mabaki yake yaliyoanguka yamewajeruhi watu watatu katika bandari ya kusini ya Odesa.
Jeshi limesema ndege nyingi zililenga mkoa wa Odesa. Wizara ya mambo ya ndani ya Ukraine imesema mabaki hayo yaligonga majengo ya makazi na kuharibu bomba la gesi.
Shambulizi hilo la ndege zisizo na rubani lilifuatiwa na mashambulizi ya makombora Jumanne ambayo yalijeruhi takriban watu 17 katika mji wa kaskazini mashariki wa Kharkiv.
Gavana wa mkoa wa Kharkiv, Oleh Synehubov, amesema kwenye mtandao waTelegram kwamba makombora mawili ya Russia, S-300 yalipiga katikati ya jiji, ikiwa ni pamoja na majengo ya makazi.
Umoja wa Mataifa umesema katika ripoti mpya Jumanne kwamba mashambulizi ya Russia, yamesababisha ongezeko la vifo vya raia nchini Ukraine kwa mwezi Disemba.