Katika mkutano na wanahabari, Al Jaber alijibu ripoti ya Desemba 3 katika gazeti la Guardian kufuatia maoni aliyoyatoa mwezi uliopita kuhusu kuondolewa kwa mafuta ghafi ambayo yamezua ukosoaji katika mkutano wa COP28.
Al-Jaber alielezea kushagazwa kwake na kile alichotaja kuwa juhudi za mara kwa mara kushutumu kazi yake kama rais wa COP 28.
Al Jaber aidha ameitaja ripoti ya Gurdian kuwa ya kupotosha baada ya taarifa ya Gurdian kumnukuu Rais huyo akisema "hakuna sayansi huko nje, au hali yoyote huko nje, ambayo inasema kwamba kuondolewa kwa mafuta ghafi ndiko kutafikia nyuzi joto 1.5.
“Nimesema mara kwa mara katika matukio mengi na katika majukwaa mengi tofauti, kwamba ni sayansi ambayo imeongoza kanuni za mkakati wetu kama rais wa COP28. Na nimekuwa wazi sana kuhusu hilo. Ninatumai kwamba wakati huu niko. wazi zaidi katika kufikisha ujumbe huu."Alisema rais huyo wa COP28
Shirika la Umoja wa Mataifa la sayansi ya hali ya hewa pamoja na Jopo la Kiserikali kuhusu mabadiliko ya hewa, limesema kupunguza ongezeko la joto hadi nyuzi joto 1.5 ifikapo mwaka 2050 kunahitaji kupunguza kwa kiasi kikubwa matumizi ya nishati ya mafuta na kuondoa matumizi ya makaa ya mawe.
Wakati huo huo mwanaharakati wa hali ya hewa wa Uganda, Vanessa Nakate alisema wakati wa COP28 kwamba mabilioni ya dola na wala sio mamilioni, yanahitajika kushughulikia mzozo wa hali ya hewa unaoendelea.
"Ninajua kwamba baadhi ya ahadi zimetolewa kuhusiana na hazina kufidia madhara na uharibifu, lakini nyingi ya ahadi hizi zimekuwa zikija kwa mamilioni. Hata hivyo, gharama za madhara na uharibifu ni mabilioni,”alisema Nakate
“Kuna watu ambao wako mstari wa mbele kushinikiza suala la mabadiliko ya hali ya hewa na wanahitaji mabilioni kushughulikia athari mbaya zaidi za janga hili na sio mamilioni.Na ninaposema kuwa fedha inapaswa kuhudumia masilahi ya watu, ni kwa sababu mabadiliko ya hali ya hewa ni zaidi ya hali ya hewa. kuliko takwimu. Ni kweli kuhusu watu. Na ndiyo maana sisi, lazima tuwe na taswira ya kibinadamu katika mazungumzo kuhusu mgogoro wa hali ya hewa."aliongeza
Mkutano wa COP 28 ambao unafikia kilele wiki ijayo unajiri wakati ambapo matukio mbaya ya hali ya hewa yameshuhudiwa kote duniani, Afrika ikiathirika zaidi.