Jeshi la Israel linaendelea na operesheni zake katika hospitali ya Al Shifa mjini Gaza

Picha iliyotolewa na IDF kuonesha operesheni za wanajeshi wake huko Gaza

Jeshi la Israel IDF, limesema Alhamisi kwamba majeshi yake yanaendelea na operesheni yake ya kijeshi katika hospitali ya Al Shifa likidai ni makao makuu ya kundi la Hamas licha ya kwamba haijagundua kitu baada ya shambulizi la Jumatano.

Katika taarifa yake Jumatano jioni kwamba baada ya wanajeshi wake kuvamia hospitali hiyo kwenye ukanda wa gaza wakati wa alfajiri Jumatano wamegundua silaha, vifaa vya mawasiliano na ujasusi vya Hamas.

Lakini wizara ya afya inayongozwa na Hamas imesema kwamba wanajeshi wa Israel hawakugundua silaha zezote kwenye hospitali hiyo.

Munir al-Boursh afisa muandamizi wa wizara afya ya Gaza amesema kwamba wanajeshi wa Israel walingia katika gorofa ya chini ya hospitali na kupekua kila kitu katika jengo la Al Shifa ikiwa ni pamoja na idara za dharura na upasuaji.

Nje ya hospitali ya Al Shifa wakati jeshi la Israel likifanya operesheni ndani jengo hilo

Akizungumza kwa simu akiwa ndani ya hospitali jumatano mchana alisema wanajeshi wangali ndani ya jengo na wanawake na watoto wanauwoga mkubwa.

Hakuna uwezo wa kuthibitisha na kufahamu kwa njia huru jinsi hali iliyokua ndani ya hospitali hiyo.

Israel haijatoa picha wala video kuthibitisha madai yao ya kuwepo kwa makamo makuu ya wanamgambo wa Hamas kwenye hospitali ya Al Shifa. Hamas na maafisa wa hospitali wanakanusha tuhuma hizo.

Akizungumza na waandishi habari baada ya mazungumzo yake na rais wa China XI Jinping, Rais Joe Biden wa Marekani alisema wanauhakika Hamas inamakao makuu yake chini ya hospitali pamoja na silaha.