Widodo yuko Washington kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia kufikia kiwango cha Mshirika kamili wa Usalama na Ulinzi, viwango vya juu kabisa vya kidiplomasia vya Marekani.
Akizungumza kabla ya mkutano wake na Biden katika Ikulu, Widodo alisema nchi yake ina matumaini ushirikiano huo mpya utachangia katika amani ya kikanda na kimataifa.
Hivyo aliendelea kusema kwamba “Indonesia inatoa wito kwa Marekani kufanya juhudi zaidi kusitisha mateso huko Gaza,” akiongeza kwamba “usitishaji mapigano ni lazima ufanyike kwa ajili ya ubinadamu.”
Biden alitaja orodha ya mambo yenye maslahi ya pamoja ikiwa ni pamoja na ushirikiano wa usalama katika usafiri wa baharini, kujenga mfumo thabiti wa uchukuzi wa bidhaa, na mpito kuelekea nishati mbadala ili kupambana na mzozo wa hali ya hewa.
Hakutaja suala la vita vya Gaza. Lakini baadae aliitaka Israel kuchukua tahadhari zaidi katika kuwalinda raia.
Viongozi hao wawili wanatofautiana kabisa juu ya ugomvi huo, pale Biden akiunga mkono Israel bila ya kutetereka na Widodo akidai kusitishwa mara moja mapigano huko Gaza.
Widodo anaunga mkono pia tume ya Umoja wa Mataifa ambayo imekua ikikusanya ushahdii wa uhalifu wa vita unaotendwa na pande zote mbili tangu shambulio la Hamas la Oktoba 7.