Rais Biden, alijaribu kueleza hoja ya kujihusisha zaidi kwa Marekani katika nchi hizo mbili akisema kwamba "ikiwa uvamizi wa kimataifa utaruhusiwa migogoro na ghasia zitaweza kuenea katika sehemu nyingine za dunia."
"Hamas na Putin wanawakilisha vitisho tofauti," alisema Biden. "Lakini wanamalengo ya pamoja. Wote wanataka kuangamiza taifa jirani la kidemokrasia."
Amesema atawasilisha pendekezo la kuhitaji fedha za dharura mbele ya Bunge, ambayo inatarajiwa kufikia dola bilioni 100, kwa kipindi cha mwaka mmoja ujao. Pendekezo hilo, ambalo litatangazwa Ijumaa, ni pamoja na fedha kwa ajili ya Ukraine, Israel, Taiwan na usimamizi wa mpaka wa kusini mwa Marekani.
"Ni uwekezaji wa busara, ambao utazaa matunda kwa usalama wa Marekani kwa vizazi vijao," alisema Biden.
Biden ana matumaini kwamba kuchanganyisha masuala hayo yote katika mswaada mmoja wa sheria utaweza kubuni muungano wa kisiasa unaohitajika ili kuweza kuidhinishwa na bunge.
Hotuba yake imetolewa siku moja baada ya safari yake muhimu huko Israel ambako alionyesha uungaji mkono kwa nchi hiyo katika vita vyake na Hamas huku akihimiza kupelekwa kwa msaada wa dharura kwa Wapalestina kwenye Ukanda wa Gaza.
Biden hali kadhalika alitoa wito kwa Wamarekani kuweka kando ugomvi kati yao na chuki ikiwa ni dhidi ya Waislamu, Mayahudi au watu wengine kwa ajili ya maslahi ya umoja wa nchi.
Kiongozi huyo wa Marekani alirudia msimamo wa kuunda mataifa mawili ya Israel na Plaestina yanayoishi kama majirani wema kwa amani.