Mkuu wa jeshi la Sudan alisema Ijumaa kuwa hakuomba msaada wa kijeshi katika ziara ya hivi karibuni ya kikanda na kwamba anapendelea kutafuta suluhu ya amani kwa mzozo ambao umesababisha vifo vya maelfu na mamilioni ya raia kukimbia makazi yao.
Jenerali Abdel Fattah al-Burhan pia alisema katika mahojiano na shirika la habari la Reuters kwamba ameyataka mataifa jirani kuacha kutuma mamluki kukiunga mkono Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF).
Vita kati ya jeshi na RSF vilizuka katikati ya mwezi Aprili kuhusu mipango ya mpito wa kisiasa na kuingizwa kwa kikosi cha RSF katika jeshi, miaka minne baada ya mtawala wa muda mrefu Omar al-Bashir kupinduliwa katika mapinduzi ya wananchi.
Kila vita huisha kwa amani, iwe kwa mazungumzo au kwa nguvu. Tunaendelea na njia hizo mbili, na njia tunayopendelea ni njia ya mazungumzo, Burhan alisema pembeni ya Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa huko New York.