Hayo yalijiri wakati maandamano ya kuunga mkono uongozi wa kijeshi yakifanyika nje ya Ubalozi wa Ufaransa katika mji mkuu wa Niger, Niamey, kufuatia mapinduzi ya kijeshi ya wiki iliyopita.
"Rais Macron hatavumilia shambulio lolote dhidi ya Ufaransa na maslahi yake," afisi yake ilisema katika taarifa yake, ikibainisha kwamba itajibu mashambulizi dhidi ya wanadiplomasia wa Ufaransa, vikosi vyake au biashara.
Macron alizungumza na Rais wa Niger aliyeondolewa madarakani Mohamed Bazoum na rais wa zamani wa nchi hiyo, Mahamadou Issoufou, taarifa hiyo ilisema, na kuongeza kuwa wote wawili walilaani mapinduzi hayo na kutoa wito wa utulivu.
Ufaransa ilitangaza Jumamosi kuwa inasitisha misaada yote ya maendeleo kwa Niger na kutoa wito wa kurejeshwa kwa Bazoum madarakani. Niger imekuwa mshirika wa usalama wa Ufaransa, na Marekani, ambazo zimeitumia nchi hiyo kama kituo cha kupambana na waasi wa Kiislamu katika eneo pana la Sahel la Afrika Magharibi na Kati.