Mkutano huo uliongozwa na Rais William Ruto wa Kenya kama mpatanishi wa IGAD na kujadili pia juu ya uwezo wa kupelekwa kikosi cha dharura cha kikanda ili kudumisha amani.
Wakikutana mjini Addis Ababa mjni mkuu wa Ethiopia, viongozi wa Kenya, na Ethiopia pamoja na mawaziri wa mambo ya nje wa Djibouti, Somalia na Uganda, pamoja na wajumbe wa Marekani, Umoja wa Mataifa, na wa serikali ya mpito ya kiraia ya Sudan iliyopinduliwa na wanajeshi, wametaka pande zote mbili kusitisha mapigano na kuanza mazungumzo ya amani mara moja.
Akifungua mkutano rais Ruto amesema viongozi wa kijeshi wa pande zote mbili wanalazimika kusitisha mapigano bila ya masharti na kuanza mazungumzo.
"Mkutano huu lazima ufungue njia ili kuweza kupatikana makubaliano yasiyo na masharti ya kusitisha mapigano ambayo yataruhusu kuwasilishwa kwa msaada wa dharura bila ya pingamizi yoyote, kuhakikisha usalama wa raia, kusitisha uharibifu wa mali na miundombinu pamoja na kukomesha mauaji ya binadamu, na hivyo kuwawezesha wasudan kupata huduma za kijamii," alisema rais Ruto.
Kiongozi wa Kenya amependekeza masuala matatu muhimu ili kuweza kurudisha amani nchini Sudan. Moja ni kuruhusu msaada wa dharura kufika kila mahala bila ya vizuizi, pili kuanzisha maungumzo ya moja kwa moja kati ya viongozi wa jeshi la Sudan na kikosi cha RSF, na tatu kupanga mazungumzo ya kitaifa yatakayowahusisha watu wote ili kutayarisha mpito kuelekea demokrasia nchini humo.
Hata hivyo serekali ya kijeshi ya Sudan haijapeleka ujumbe wake huko Addis Ababa ikisema kwamba ombi lao la kumondoa rais Ruto kama mpatanishi halijatiliwa maanani. Ujumbe wa kikosi cha dharura cha Sudan RSF unahudhuria mkutano huo.
Taarifa ya IGAD kuhusu mkutano huo inasema kwamba wajumbe waliokutana Addis Ababa wametaka mkutano mwingine wa viongozi uitishwe ili kuzungumzia suala la kupelekwa kikosi cha dharura cha Jumuia ya Afrika Mashariki.
Akiikaribisha kamati hiyo, waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed ametahadharisha kwamba bila ya suluhihso la haraka, ugomvi huo unaweza kusambaa na kuhatarisha usalama wa kanda nzima.
"Ni karibu wiki 12 sasa tangu kuanza kwa mapigano ya Sudan kati ya jeshi la taifa la Sudan na kikosi cha dharura cha RSF. Tunakutana hapa leo ili kutathmini hali ya mambo kutokana na mzozo huu mbaya ambao unaendelea kuzusha wasi wasi mkubwa muda unapoendelea. Na tumekutana hapa ili kutafuta njia na namna ya kukomesha uharibifu huu mbaya na kutafuta makubaliano ya kuwepo maelewano ya kudumu na ya kukomesha uhasama," alisema Abiy
Juhudi za kidiplomasia na mazungumzo ya Riyadh yaliosimamiwa na Marekani na Saudi Arabia yalisitishwa mwezi uliopita baada ya kushindwa kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano.
Misri nayo imetangaza kwamba itaitisha mkutano wa viongozi wa mataifa jirani ya Sudan hapo Julai 13 kujadili njia za kumaliza mzozo huo.
Taarifa ya IGAD kadhalika imesema kwamba kwa ushirikiano na Umoja wa Afrika, wataanzisha utaratibu wa mazungumzo kuwahusisha raia kwa lengo la kutafuta amani nchini Sudan.