Putin apinga mpango wa amani na Ukraine ulowasilishwa na viongozi wa Afrika

  • Abdushakur Aboud

Rais Vladimir Putin anawaonesha viongozi wa Afrika masuala asiyokubaliana nayo kwenye mpango wa amani.

Rais Vladimir Putin amepinga mpango wa amani ambao viongozi wa nchi za Afrika walikua na matumaini utaweza kumaliza vita na Ukraine, walipokutana nae mjini St. Petersburg, siku ya Jumamosi.

Viongozi kutoka nchi saba za Afrika walimuambia Putin kwamba, vita vinadhuru dunia nzima. Ujumbe huo ulikutana na Putin siku moja baada ya kukutana na rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky mjini Kyiv.

Putin alifungua mkutano wa Jumamosi na ujumbe wa viongozi kutoka Comoros, Jamhuri ya Congo, Afrika Kusini, Misri, Senegal, Afrika Kusini, Uganda na Zambia katika kasri moja mjini St. Petersburg, kwa kusisistiza dhamira ya Rashia kufanya kazi na nchi za Afrika.

Rais Vladimir Putin akutana na ujumbe wa viongozi wa nchi za Afrika mjini Saint Petersburg

Lakini kabla ya viongozi wote kumaliza hotuba zao Putin aliingilia kati na kupinga mpango wao wa amani, unaomtaka atambuwe mipaka ya Ukraine inayotambulika kimataifa. Alirudia msimamo wake kwamba Ukraine na washirika wake wa Magharibi ndio walianzisha ugomvi huo muda mrefu kabla ya hata Rashia kuivamia Ukraine Februari 2022.

Putin pia alisema kwamba, nchi za Magharibi ndizo za kulaumiwa kwa kuongezeka sana bei za chakula duniani tangu mapema mwaka jana, na kwamba Afrika ndio imedhurika zaidi.

Aliuambia ujumbe huo kwamba usafirishaji wa nafaka za Ukraine kutoka bahari ya Black Sea haitosaidia kamwe kupunguza matatizo ya bei za juu za chakula barani Afrika, kwa sababu sehemu kubwa ya nafaka hizo inapelekwa katika nchi tajiri.

Zelensky alipinga sehemu kubwa ya mpango huo alipokutana na viongozi hao wa Afrika siku ya Ijuma mjini Kyiv.

Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine akutana na ujumbe wa viongozi wa Afrika Mjini Kyiv, Ukraine.

Kiongozi wa Ukraine aliuambia ujumbe huo kwamba, kabla ya kuanza mazungumzo yeyote ya amani ni lazima Rashia iwaondoe wanajeshi wake wote kutoka ardhi ya Ukraine, jambo ambalo Moscow imesema haliweza kukubalika.

Putin anasema Rashia haijapata kukata mazungumzo, lakini ni Kyiv ndio imezuia mazungumzo kuendelea. Anasema mazungumzo yanabidi kutilia maanani "ukweli uliopo" hii leo, kutambua kukaliwa kwa majimbo matano ya Ukraine na Rashia ambapo manne haina udhibiti kamili. Kyiv hakubaliani na sharti hilo.