Katibu mkuu UM ataka kusimamishwa mapigano na msaada kwa Sudan

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, Jumatano ametoa mwito wa kumalizika kwa mapigano nchini Sudan, na msaada wa kimataifa kwa watu wa Sudan ambao amesema wanakabiliwa na janga la kibinadamu.

“Misaada lazima iruhusiwe kuingia Sudan, na tunahitaji njia salama na kuwezeshwa kwa haraka kusambazwa kwa watu wanaoihitaji sana,” alisema katibu mkuu Gutteres wakati wa mkutano na wanahabari jijini Nairobi, Kenya.

Ameongeza kusema kwamba raia na miundombinu ya kiraia lazima ilindwe, na wafanyakazi wa misaada ya kibinadamu, na mali zao zinapaswa kuheshimiwa.

Wizara ya afya ya Sudan inasema watu 500 wameuwawa, na takriban 5,000 wamejeruhiwa toka mapigano kuanza hapo Aprili 15, baada ya mapambano ya madaraka kuzuka baina ya viongozi wa vikosi vya serekali ya Sudan, na wanamgambo wa akiba.

Shirika la uhamiaji la Umoja wa Mataifa (IOM) limesema wiki hii watu 334,000 wamehama makazi yao ndani ya nchi kutokana na mapigano ikiwa ni nyongeza ya watu 100,000 ambao wamekimbilia nje ya nchi.