Kuendelea kuimarika kwa mahusiano baina ya Riyadh na Tehran baada ya miaka kadhaa ya kutoaminiana kulionekana Jumatatu pale Saudi Arabia iliposaidia kuwaondoa raia wa Iran kutoka Sudan ambako kuna vita kwa sasa.
Jeshi la Sudan la wanamaji liliwabeba raia 65 wa Iran kutoka Port Sudan mpaka Jeddah, ambapo watasafirishwa mpaka Tehran.
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Iran, Nasser Kanani ameita hatua hiyo iliyochukuliwa kuwa yenye ishara njema na kuishukuru Saudia kwa ushirikiano.
Ahmed al-Dabis, afisa wa ngazi ya juu wa Saudi Arabia, amewaeleza raia wa Iran walioondolewa Sudan katika video iliyo rushwa na televisheni ya huko kwamba mataifa hayo mawili yalikuwa marafiki wakubwa, ndugu na wanapaswa kuiona falme hiyo kama nyumbani.
Saudi Arabia iliyo upande wa pili wa bahari ya sham kutokea Sudan, imekuwa ni kituo muhimu kwa juhudi za uokozi wakati mataifa yanajitahidi kuondoa maelfu ya raia wa kigeni kutoka Sudan yenye mgogoro ulioanza Aprili 15.