Rais wa Iran kwenda Syria Jumatano

Rais wa Iran, Ebrahim Raisi, atasafiri kwenda  Damascus Jumatano, vyombo vya habari vya serikali ya Iran vimeripoti vikitangaza ziara hiyo ya siku mbili kuwa ni muhimu sana kwa ushirikiano wa kikanda na utawala wa Syria.

Ziara ya rais Raisi, mjini Damascus, ni muhimu sana kutokana na mabadiliko na maendeleo ya eneo hilo shirika la habari la IRNA Jumapili limemnukuu balozi wa Iran nchini Syria, Hossein Akbari akisema hayo.

Kwa mujibu wa IRNA, Raisi ataongoza ujumbe wa juu wa kiuchumi na kisiasa katika safari yake ya siku mbili kwa mwaliko rasmi wa Rais wa Syria Bashar al-Assad.

Tehran, mshirika mkuu wa Assad, ameiunga mkono serikali yake wakati wa mzozo wa miaka 12 wa Syria, lakini hakuna rais wa Iran aliyetembelea huko tangu vita vilipoanza 2011.

Ziara hiyo inakuja wiki kadhaa baada ya makubaliano ya kihistoria ya maelewano kati ya wapinzani wa kikanda Iran na Saudi Arabia, ambayo pia yamesisitiza nia kubwa ya Waarabu kushirikiana tena na serikali ya Syria iliyokuwa imetengwa.