Ujerumani yalaani ghasia za mwaka mpya

Serikali ya Ujerumani Jumatatu ililaani matukio ya mkesha wa mwaka mpya ambapo maafisa wa polisi na wafanyakazi wa zima moto walishambuliwa, hasa kwa fataki.

Watu kote Ujerumani Jumamosi walianza tena utamaduni wao wa kufyatua fataki nyingi katika maeneo ya umma ili kuukaribisha mwaka mpya.

Matukio kama hayo yalipigwa marufuku kwa miaka miwili iliyopita ikiwa ni juhudi za kukabiliana na janga la COVID-19.

Sherehe mwaka huu ziliambatana na idadi kubwa ya ghasia ambapo maafisa wa dharura walivamiwa kwa fataki.

Mjini Berlin, kikosi cha zimamoto kilihesabu takriban mashambulizi 38 ya aina hiyo na kusema maafisa 15 walijeruhiwa.

Kwa upande wa polisi, wenyewe walisema walikuwa na maafisa 18 waliojeruhiwa, kwa mujibu wa ripoti za shirika la habari la Ujerumani DPA.