Wamarekani washauriwa kubaki nyumbani kutokana na baridi kali na theluji nyingi

  • Abdushakur Aboud

Lori la kusafirisha bidhaa lakwama barabarani Ontario, Canada kutokana na theluji na baridi kali.

Mamilioni ya wamarekani wamelazimika kufutilia mbali mipango ya kusherehekea siku kuu ya Krismasi kutokana na baridi kali kuwahi kushuhudiwa baada ya miongo kadhaa, huku maafisa wa serikali katika majimbo mengi wakiwashauri watu kubaki majumbani.

Upepo mkali na theluji katika miji kuanzia kaskazini hadi kusini mwa Marekani umesababisha usafiri wa ndege kuwa mgumu na mashirika ya ndege kufuta karibu safari 5 700 za ndege siku ya Ijuma pekee yake.

Wasafiri wasubiri kuandikishwa kusafiri katika ukumbi wa United Airlines kabla ya Krismasi kwenye uwanja wa O'Hare Chicago, Marekani

Rais Joe Biden akizungumza na waandishi habari siku ya Alhamisi aliwaonya Wamarekani kuchukua tahadhari kutokana na baridi kali na kusafiri mapema ikiwa wana mipango ya kukusanyika pamoja na familia na marafiki kwa ajili ya Krismasi.

Rais Joe Biden wa Marekani azungumza kutahadharisha wakazi juu ya dharuba kali ya baridi inayokumba Marekani kabla ya Krismasi.

Rais Biden amebaki Washington kusherehekea Krismasi amesema hali ni ya hatari na kwamba amezungumza na maafisa wa Mamlaka ya Huduma za Dharura, FEMA, na Idara ya Taifa ya Hali ya Hewa juu ya mipango yao.

Hali hii ya hewa ambayo ni nadra na hutokea mara moja katika kizazi kulingana na watabiri wa hali ya hewa, imeathiri majimbo 26 ya Marekani kutokana na upepo mkali wa baridi unaokwenda kwa kasi ya kilomita 100 kwa saa hadi kufikia mpaka wa Mexico upande wa Kusini.

Hali hii imesababisha pia mafuriko na theluji nyingi katika majimbo ya kaskazini na baridi ya kugandisha maji inakumba majimbo ya mashariki na kuwaathiri watu milioni 240.

Watu 12 wameripotiwa wamefariki kutokana na baridi kali huku miji ikifungua vituo maalum kwa ajili ya watu wasio na makazi wanaoishi barabarani.

Wateja wakaidi hali mbaya ya hewa kutokana na dharuba ya theluji mjini Birmingham, Michigan.

Karibu watu milioni 1.8 hawana umeme katika nusu ya majimbo ya mashariki pamoja na Texas siku ya Jumamosi kutokana na dhoruba kali, ambapo majimbo ya kusini yakiathirika zaidi.

Baridi hii kali inayotokea Bara la Arctic, inaiathiri pia Canada ambako shughuli nyingi zimesita kutokana na theluji nyingi kuwahi kutokea.