Timu ya taifa ya Senegal maarufu kama Simba wa Teranga wanaanza kampeni yao kuwania ubingwa wa kombe la dunia huko Qatar kwa kupambana na uholanzi huku wakimkosa mcheza kandanda bora wa kiafrika mwaka 2022, Sadio Mane ambaye ni mmoja wa washambuliaji hatari sana duniani katika timu ya Bayern Munich. Mchango wake ulikuwa muhimu sana kwa mafanikio ya timu ya taifa ya Senegal mwaka huu, ushahidi uliobainika katika mchezo wa fainali ambapo uliipatia ushindi katika mikwaju ya penati na kuishinda Misri mwezi Februari katika fainali za kombe la mataifa ya Afrika. Jinamizi la mashabiki wa Senegal lilijitokeza Alhamisi wiki iliyopita wakati timu ilipotangaza kuwa mchezaji Sadio mane atakosa mechi za Kombe la Dunia akihitaji kufanyiwa operesheni kutokana na majeraha aliyopata.