Russia yahamisha 70,000 kutokana na wasiwasi wa shambulio la Ukraine la kulipiza kisasi

Muonekano unaonyesha jengo la jumba la mazoezi lililoharibiwa na shambulio la kombora la Russia huko Mykolaiv, Ukraine Novemba 1, 2022. REUTERS

Russia imeamuru  maelfu ya raia wa Ukraine wanaoishi karibu na ukingo wa mashariki wa Mto Dnipro kuhama, agizo ambalo Kyiv inasema ni sawa na "kulazimika kupoteza  makazi yao."

Mamlaka zilizowekwa na Russia ziliripoti kuwahamisha wakazi 70,000 kutokana na wasiwasi wa shambulio kubwa la Ukraine la kulipiza kisasi.

Russia inaendelea kulenga nyumba za raia na miundombinu muhimu, ikirusha makombora manne usiku kucha ambayo yalibomoa nusu ya jengo la ghorofa katika mji wa bandari wa Myko-laiv.

Russia ilirusha darzeni ya makombora katika vituo vya nishati vya Ukraine siku ya Jumatatu, na kusababisha kukatika kwa umeme, uhaba wa maji na kukatika kwa huduma za simu za mkononi.

Akizungumza na waandishi wa habari katika Wizara ya Mambo ya Nje siku ya Jumanne, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje Ned Price alilaani mashambulizi hayo na kusema Russia ilirusha takriban makombora 100 siku ya Jumatatu na Jumanne.