Kauli hii imetolewa mjini Kigali wakati wa ufunguzi wa mkutano wa siku nne unaahudhuriwa na viongozi wakuu wakiwemo marais na wakuu wa serikali.
Africa Green Revolution Forum ni mkutano mkubwa ambao unazungumzia umuhimu wa waafrika katika bara hilo kushirikiana ili kukabiliana na changamoto zinazopatikana kwenye mfumo mzima wa uzalishaji chakula barani Afrika.
Wajumbe wengi wanaohudhuria mkutano huu ni viongozi wenye sauti katika nyanja mbalimbali zikiwemo serikali na mashirika ya kimataifa kuhusu kilimo,uwekezaji na fedha lakini wote kwa pamoja wamesema kwamba kwa kawaida Afrika imekuwa na changamoto kwenye suala zima la uzalishaji wa chakula cha kutosha. Lakini kwa wakati huu dunia inapokabiliwa na mizozo ya kivita maafa na mabadiliko ya hali hewa hali imezidi kuwa mbaya.
Haile Mariam Desalegne aliwahi kuwa waziri mkuu wa Ethiopia, kwa sasa ni mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi wa AGRF jukwaa la kilimo na chakula Afrika anasema kwamba mikakati ya haraka inahitajika
‘’Tunaihitaji sasa hivi tofauti na hilo Afrika itakuwa kwenye hatari kubwa ya kuwa bara pekee duniani litakalokuwa na baa la njaa ifikapo mwaka 2030. Uwiano wa bei ya vyakula umepanda na kufikia kwenye cha asilimia 42 tangu kuripuka kwa janga la Covid-19. Na kwa kuendelea kuwepo na athari za mabadiliko ya hali ya hewa, mafanikio madogo yaliyokuwa yamepatikana kwa usalama wa chakula yanaendelea kudidimia kwa namna mahsusi katika bara letu la Afrika,’’ anasema Haile Mariam.
Mkutano huu unafanyika ikiwa zimebaki takribani siku chache kabla mkutano wa baraza kuu la Umoja wa Mataifa, na wadau wanasema Afrika inatakiwa kwenda kwenye mkutano huo wakiwa na sauti moja. Dr Agnes Kalibata ni mkurugenzi mkuu wa jukwaa hili la kilimo na chakula maarufu kama AGRF.
‘’Wiki hii kuhusu mgogoro wa chakula inakuja kwenye maandalizi ya mkutano wa baraza kuu la Umoja wa Mataifa na watu watalizungumzia jambo hili, tunataka Afrika iwe na msimamo wake kabla ya kwenda kwenye mkutano huu. Wakati tukijiandaa na mkutano wa mazingira wa COP 27 ambapo tunazungumzia uthabiti wa mfumo wa mazingira, sisi katika mkutano huu tunachukua msimamo gani? Tuchukue nafasi hii kama fursa ya sisi waafrika kuwa na msimamo wa pamoja wa jinsi gani tunakwenda kujikwamua kwenye migogoro hii,’’ anasema Dr. Agnes Kalibata.
Rwanda ambayo ni mwenyeji wa mkutano huu imesema kwamba "ili mikakati hii ifanikiwe ni lazima kila nchi na serikali kulifanya suala la usalama wa chakula,mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa liwe kipaumbele katika kuleta suluhu ya matatizo haya". Waziri mkuu wa Rwanda Dr Edouard Ngirente alisema.
Rais Paul Kagame anasema ‘’kwa kuwa tunajadili mfumo wa chakula ngoja niwape taarifa kuhusu kile tunachokifanya sisi kama Rwanda kwa kifupi, tangu mwaka 2008 wakati wa msukosuko wa kiuchumi Rwanda imewekeza kwa kiasi kikubwa kwenye matumizi ya teknolojia kwenye kilimo cha kisasa. Na tunapojitahidi kufikia lengo la usalama wa chakula Rwanda inaendelea kuweka nguvu kwenye mikakati mingine.’’
Mkutano huu wa siku nne unahudhuriwa na marais wa nchi,manaibu rais, viongozi wa zamani serikalini pamoja na wakurugenzi wakuu wa mashirika ya fedha ulimwenguni. Tanzania imewakilishwa na makamu wake wa Rais Dr. Phillip Isdor Mpango.
Sylivanus Karemera Sauti ya Amerika-Kigali