Ripoti ya Umoja wa Mataifa yawahusisha askari wa Mali na Wagner katika mauaji ya raia

Wanajeshi wa Mali wakipiga doria na wanajeshi wa Ufaransa katika mji wa Menaka, Mali

Wanajeshi wa serikali ya Mali na "wanajeshi wazungu" waliwakamata raia 33 katikati mwa Mali mwezi Machi ambao baadaye walikutwa wakiwa wamepigwa risasi na miili yao kuchomwa moto, wachunguzi   wa vikwazo wameliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa .

Ripoti hiyo haiwataji wanajeshi hao “wazungu" ambao wanatuhumiwa kuwakamata wanaume na wavulana wakubwa katika kijiji kidogo cha Mali, kuwafunga mikono nyuma ya migongo yao na kuwafunika macho. Wanajeshi wa Mali baadaye waliwasili na wanatuhumiwa kuwapiga watu hao na kuwachukua raia wa Mauritania 29 na raia wa Mali wanne.

Wanawake walisubiri kurejea kwa wanaume hao, lakini walijulishwa na jamaa zao siku moja baadaye kwamba miili ya wanaume hao imepatikana umbali wa kilomita 4 . Wanaume hao walikuwa wamepigwa risasi na kisha kuchomwa moto, waliandika wachunguzi wa Umoja wa Mataifa, wakinukuu ushuhuda waliopokea.

Kundi la Wagner la Russia lilianza kusambaza mamia ya wapiganaji mwaka jana kulisaidia jeshi la Mali na tangu wakati huo limelaumiwa na mashirika ya kutetea haki za binadamu na wakaazi wa eneo hilo kwa kushiriki katika mauaji ya raia.

Serikali ya Russia imekiri wafanyakazi wa Wagner wako nchini Mali, lakini serikali ya Mali imewataja kama wakufunzi kutoka jeshi la Russia na siyo wakandarasi binafsi wa usalama. Wagner hawana wasemaji na hawajazungumzia shutuma za ukiukaji wa haki za binadamu.