Ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Uganda hadi Tanzania upo matatani

Rais wa Uganda Yoweri Museveni akiwa na mwenzake wa Tanzania Samia Suluhu Hassan walipokutana katika ikulu ya Entebbe April 11, 2021

Deutsche Bank imeripotiwa kwamba haitafadhili mradi mkubwa wa ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Hoina Uganda hadi Tanga, Tanzania.

Hii ni baada ya wanaharakati wa mazingira kuasilisha malalamiko kwamba ujenzi wa bomba hilo utasababisha baadhi ya watu kupoteza makazi yao, pamoja na kuvuruga maisha ya wanyama wa porini.

Shirika la habari la Reuters limeripoti kwamba benki hiyo kubwa ya Ujerumani imekumbana na shinkizo kubwa kutaka kueleza mkataba wake wa ufadhili wa mradi huo wa ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta, utakaogharimu kiasi cha dola bilioni 3.5.

Bomba hilo lina urefu wa kilomita 1,400, kati ya Uganda na Tanzania.

Benki ya Deutsche haijatoa taarifa kamili lakini kundi la kutetea mazingira la 350.org linapanga maandamano kupinga ufadhili wake katika siku zijazo.

Kundi hilo limesema kwamba wafadhili kadhaa wa mradi huo na mashirika ya bima yamejiondoa na sasa wanataka benki ya Deutsche kujiondoa.