Polisi wa Afrika kusini Jumatatu wamesema wamemfungulia mashtaka mtu mmoja kwa kosa la uchomaji moto uliosababisha uharibifu mkubwa katika jengo la bunge la taifa mjini Cape Town, huku zima moto wakijaribu kuzima mabaki ya moto huo.
Moto huo ulizuka mapema Jumapili katika ukumbi wa bunge, ambao baadhi ya sehemu zake zilijengwa mwaka 1884 na unajumuisha bunge la taifa.
Moto huo ulisabisha kuporomoka kwa paa la jengo la baraza la Seneti Jumapili na kuharibu sakafu nzima, ingawa hakukuwa ripoti za mtu yeyote kujeruhiwa katika tukio hilo.
Mshukiwa mwenye umri wa miaka 49 aliyekamatwa kuhusiana na moto huo anatarajiwa kufikishwa mahakamani kesho Jumanne na atakabiliwa na mashtaka ya kuvunja nyumba na wizi pamoja na uchomaji moto, kitengo maalam cha polisi kijulikanacho kama Hawks kimesema katika taarifa.