Maagizo hayo yanaeleza kuwa ili kuingia ndani ya basi, kwenye migahawa na baa, kanisani na msikitini, lazima uwe umepata chanjo kamili ya Covid 19.
Serikali inasema imechukua hatua hizo ili kuzuia ongezeko la maambukizi ya corona ambalo limeshuhudiwa hivi karibuni, likichochewa na aina mpya ya kirusi cha Omicron ambacho kinaambukiza kwa kasi.
Uchumi wa Rwanda unategemea kwa asilimia 48 huduma za umma pamoja na utalii, kwa hiyo kulikuwa umuhimu wa kuchukua hatua madhubuti ili uchumi usiendelee kudidimia kutokana na kusambaa kwa virusi vya corona, wanasema wachambuzi wa masuala ya uchumi.
Hata uwekezaji wa moja kwa moja kutoka nje ambao unachangia sana kwenye uchumi wa nchi umepungua sana katika kipindi hiki cha janga la Covid 19.
Kulingana na taasisi ya Umoja wa mataifa inayofuatilia masuala ya biashara na uwekezaji ( UNCTAD), uwekezaji wa kutoka nje kuelekea Rwanda ulitoka kwenye dola milioni 354 mwaka 2019 na kushuka hadi dola milioni 135 mwaka 2020, kutokana na mzozo wa kiuchumi duniani uliosababishwa na janga la Covid 19.