Kongamano la kuisaidia Afghanistan kifedha laandaliwa Pakistan

Kongamano maalum kuhusu Afghanistan nchini Pakistan

Mkutano wa dharura wa nchi 57 wanachama wa muungano wa ushirikiano wa nchi za Kiislamu OIC, uliochukua siku nzima, umekubaliana kuunda mfuko maalum utakaochangisha pesa kwa ajili ya kushughulikia mgogoro wa kibinadamu na kiuchumi nchini Afghanistan, ambapo mamilioni ya watu wanakabiliwa na uhaba wa chakula huku kiasi cha watoto milioni moja wapo kwenye hatari ya kufariki kutokana na utapia mlo uliokithiri.

Taarifa kutoka kwa washiriki wa mkutano huo uliofanyika Pakistan, imesema kwamba pesa hizo zitachangishwa kwa kuwajumuisha washirika wa maendeleo na kupitia kwa benki ya maendeleo ya kiislamu.

Kongamano hilo liliwahusisha wawakilishi wa Marekani, China, Russia, umoja wa ulaya na umoja wa mataifa, likiwa ndiyo kongamano kubwa zaidi kuwahi kuandaliwa kwa ajili ya kuisaidia Afghanistan tangu Taliban walipochukua madaraka kutoka kwa serikali iliyokuwa ikiungwa mkono na nchi za magharibi kutokana na hatua ya wanajeshi wa kigeni wakiongozwa na Marekani, kuondoka Afghanistan baada ya miaka 20.