Jeshi la Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), na washirika wake wa Uganda, Jumapili wamesema wamefanikiwa kuharibu ngome muhimu za waasi katika eneo la mashariki mwa DRC wiki hii katika kampeni iliyoanzishwa mwezi uliopita dhidi ya waasi wa ADF.
Vikosi kutoka mataifa mawili vilishambulia kambi mpya za adui zilizopo katika mji wa Beni, kwenye jimbo la Kivu Kaskazini na jimbo la Ituri lililopo kaskazini mwa DRC, kwa mujibu wa taarifa ya jeshi la Congo kupitia ujumbe wa Twitter.
Toka kuanzishwa kwa oparesheni ya pamoja Novemba 30, wanajeshi wamefanikiwa kuboresha barabara za eneo hilo na kuviwezesha vikosi kusafiri kwa urahisi.
Jeshi limesema limeshambulia maeneo ya waasi wa ADF wanaoshutumiwa kufanya mauaji mashariki mwa DRC, na milipuko ya mabomu nchini Uganda.