Idadi ya waandishi wa habari wanaokamatwa inaendelea kuongezeka duniani

Mwandishi wa habari wa Japan uki Katazumi akiwa ameinua mikono baada ya kukamatwa na polisi May 14 2021

Jumla ya waandishi wa habari 488 wanazuiliwa katika magereza mbali mbali kote duniani.

Hii ni idadi ya juu zaidi kuripotiwa tangu muungano wa waandishi wa habari wasiokuwa na mipaka walipoanza kuhesabu idadi ya waandishi wa habari wanaokamatwa na kuzuiliwa, miaka 25 iliyopita.

Waandishi wa habari 46 waliuawa mwaka huu, ikiwa ni idadi ndogo sana tangu muungano huo ulipoanza kuhesabu matukio yanayowahusu waandishi wa habari.

Idadi kubwa ya waandishi waliouawa wako mashariki ya kati kutokana na migogoro inayoendelea huko.

Katika taarifa, shirika hilo lisilo la kiserikali la waandishi wasiokuwa na mipaka limesema kwamba idadi ya waandishi wa habari wanaozuiliwa haijawahai kuwa ya juu namna ilivyo sasa.

Idadi imeongezeka kwa asilimia 20 katika muda wa mwaka mmoja kutokana na msako unaofanywa na maafisa wa usalama nchini Myanmar, Belarus na Hong Kong.

"Cha kushangaza sana katika hii ripoti yam waka 2021, ni idadi ya waandishi wa habari waliokamatwa na kuzuiliwa ambayo imefikia rekodi ya juu sana. Idadi imeongezeka kwa asilimia 20, waandishi wa habari 488 wamekamatwa na kuzuiliwa bila sababu kote duniani." amesema Christophe Deloire, katibu mkuu wa waandishi wa habari wasiokuwa na mipaka, akiongezea kwamba "Ukamataji umeongezeka katika nchi tatu -- China kwa sababu ya Hong Kong, huko Burma na Belarus ambako dikteta Alexander Lukashenko amekataa kukubali matokeo ya uchaguzi uliokumbwa na madai ya wizi wa kura na uliofuatiwa na msako mbaya."

Idadi ya waandishi wa habari wa kike wanaokamatwa pia imeongezeka na kufikia 60, ikiwa ni ongezeko la theluthi tatu ikilinganishwa na mwaka 2020.

China inaongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya waandishi wa habari wanaokamatwa na kuzuiliwa gerezani.

Waandishi 127 wanazuiliwa gerezani China kwa kile kimetajwa kama msako wa serikali dhidi ya uhuru wa habari.