Walinda amani wa Togo wauwawa Mali

Walinda amani saba kutoka taifa la Afrika magharibi la Togo wameuwawa Jumatano wakati gari lao lilipokanyaga mlipuko uliotegwa katikati ya Mali kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa, Stephane Dujarric amewaeleza wanahabari kwamba walinda amani wengine watatu kutoka Togo walijeruhiwa vibaya katika mlipuko huo katika mkoa wa Bandiagara.

Amesema kwamba walinda amani walikuwa ni sehemu ya msafara uliokuwa unasafirisha vifaa kati ya miji ya Douentza na Sevare.

Hakukuwa na taarifa za haraka kuelezea kundi lililo-husika na kutega mlipuko huo.

Togo linachangia wanajeshi wake 930 katika kikosi cha wanajeshi 16,000 cha Umoja wa Mataifa kilichopo Mali, kinacho julikana kama MINUSMA.

Kutokana na tukio hilo katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres ameshutumu vikali shambulizi hilo na kutaka serekali ya Mali kuwawajibisha walio husika.