Wasafiri wanaoingia Marekani watakabiliwa na masharti magumu ya kupimwa virusi vya covid 19, wakati nchi zaidi zimeweka masharti magumu ya usafiri kwenye mipaka yao licha ya kuwa hakuna uhakika juu ya ukali wa aina mpya ya kirusi cha Omicron na uwezo wake wa kupunguza kinga ya chanjo.
Japan na Hong Kong zimesema zitaongeza marufuku ya usafiri na Malaysia imeweka marufuku ya muda kwa wasafiri kutoka nchi zinazodaiwa kuwa katika hali ya hatari. Japan ambayo tayari imepiga marufuku wasafiri wapya wa kigeni kuingia, leo imeripoti kisa cha pili cha aina hiyo mpya ya virusi vya corona.
Shirika la afya duniani (WHO) limesema ‘marufuku hizo za usafiri hazitozuia kirusi hicho kipya kusambaa kote duniani, na zinaweka mzigo kwenye maisha na riziki za watu’, huku likiwashauri wale wasio na afya njema, walio katika hatari au walio na umri wa miaka 60 na zaidi na ambao hawachanjwa kuahirisha safari.
Uwekezaji kwenye masoko ya kimataifa umeendelea kuwa juu leo Jumatano, baada ya masoko ya hisa kuporomoka siku moja kabla kufuatia matamshi ya mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya Moderna ambaye alionyesha dukuduku juu ya ufanisi wa chanjo dhidi ya kirusi cha Omicron.
Maafisa wa afya duniani wamebaini ufanisi wa chanjo na wanazidi kutoa wito kwa watu kupata chanjo ya covid 19.