Mazungumzo ya kufufua mkataba wa nyuklia wa Iran wa mwaka wa 2015 yameanza tena leo mjini Vienna baada ya kusimamishwa kwa kipindi cha miezi mitano, na yanafanyika kwa mara ya kwanza tangu rais mpya wa Iran achukuwe hatamu za uongozi.
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa Iran Said Khatibzadeh amesema kwamba nchi yake inadhamira ya dhati ya kufikia makubaliano na mataifa ya magharibi.
Akizungumza na waandishi habari kabla ya kuanza mazungumzo ya Vienna amesema serikali ya Teheran imeonyesha nia ya kuwa tayari na kuchukulia kwa dhati mazungumzo kwa kupeleka wataalamu ili kuweza kufikia makubaliano.
Kama ilivyokuwa katika duru sita za mwanzo za mazungumzo, Marekani haishiriki moja kwa moja.
Iran itazungumza moja kwa moja na nchi nyingine zilizosaini mkataba huo wa 2015 ambazo ni Uingereza, China, Ufaransa, Rashia na Ujerumani, huku wanadiplomasia wa Umoja wa ulaya wakiendelea kujadiliana na Marekani.
La muhimu kwenye mazungumzo haya ya Vienna ni kuanzisha tena makubaliano yanayoiomba Iran kusitisha uzalishaji wa nishati ya nyuklia yake katika kipindi cha kati ya miaka 10 na 15 ili ipewe afueni ya vikwazo ilivyowekewa.