Aina mpya ya Corona ni hatari sana - WHO

Shirika la afya duniani (WHO) leo limesema aina mpya ya virusi vya corona inaweza kusambaa kote duniani, na kusababisha ongezeko la maambukizi ya corona ambayo yatasababisha athari mbaya katika baadhi ya maeneo.

WHO imezitaka nchi 194 wanachama wake kuharakisha utoaji wa chanjo kwa makundi yaliyopewa kipaumbele, katika hali ya kutarajia kuongezeka kwa idadi ya maambukizi, kuhakikisha mipango ya kukabiliana na maambukizi hayo inachukuliwa ili kudumisha huduma muhimu za afya.

WHO imesema ‘omicrom ina kiwango cha juu kisicho cha kawaida cha virusi vinavyobadilika, baadhi ya virusi hivyo vinatia wasiwasi juu ya athari zake kwenye mwelekewo wa janga la corona’.

WHO imeongeza kuwa ‘hatari ya jumla kwenye ngazi ya kimataifa inayohusiana na aina mpya ya virusi inatathminiwa kuwa ya juu sana’.

Kufikia sasa, hakuna vifo vilivyokwisha ripotiwa kutoka na kirusi hicho cha omicron, licha ya kuwa utafiti zaidi unahitajika ili kutathmini iwapo kirusi hicho kinaweza kupunguza kinga ya mwili iliyoboreshwa na chanjo pamoja na maambukizi ya awali.

Aina hiyo mpya ya virusi vya corona iliripotiwa kwa mara ya kwanza kwa WHO Novemba 24 kutoka Afrika kusini ambako maambukizi yameongezeka kwa kasi.