Marekani yatoa msaada wa dola milioni 144 kwa raia wa Afghanistan

Raia wa Afghanistan wakipit akatika soko mjini Kabul [Oct 12 2021]

Marekani imetangaza kwamba itatoa msaada wa kibinadamu wa kiasi cha dola milioni 144 kusaidia Afghanistan, ambapo mamilioni ya watu wamo katika hatari ya uhaba mkubwa wa chakula wkaati wa kipindi hiki cha baridi.

Msemaji wa baraza la usalama wa taifa Emily Horne amesema kwamba Marekani itatoa pesa hizo kwa mashirika yasiyo ya kiserikali yanayotoa msaada moja kwa moja kwa raia wa Afghanistan milioni 18.4 wakiwemo wakimbizi wa Afghanstan walio katika nchi Jirani.

Umoja wa mataifa umesema kwamba vita vibaya vya zaidi ya miongo minne na majanga yanayojitokeza, vimesababisha uhaba mkubwa wa chakula nchini Afghanistan.

Mahitaji ya msaada wa kibinadamu yameongezeka kwa kiwango kikubwa na zaidi ya nusu ya watu Afghanistan, ambao ni kiasi cha watu milioni 22.8 wanakabiliwa na tishio kubwa la njaa kuanzia mwezi Novemba.