Iran kuanza mazungumzo ya nyuklia

Iran, Jumatano ilitarajiwa kuanza mazungumzo na mataifa yenye nguvu duniani kuhusu maendeleo ya mpango wa nyuklia itakapofika mwezi Novemba.

Hakukuwa na uthibitisho wa mazungumzo mapya kutoka pande nyingine kuhusu makubaliano ya mwaka 2015 yaliyolenga kuizuia Tehran kuendeleza silaha za nyuklia.

Makubaliano hayo yanajumuisha mataifa ya Marekani, Uingereza, Ufaransa, Ujerumani, Russia, China na Umoja wa Ulaya, lakini rais wa zamani wa Marekani, Donald Trump, alijiondoa katika makubaliano hayo mwaka 2018, na kurejesha vikwazo dhidi ya Iran.

Jumatano, naibu waziri wa mambo ya nje wa Iran, Ali Bagheri, ambaye anahudumu kama mpatanishi mkuu wa Iran, wa makubaliano ya nyuklia, aliandika kupitia ujumbe wa Twitter kwamba wamekubali kufanya maridhiano kabla ya mwezi Novemba kukamilika.

Tarehe halisi itatangazwa katika kipindi cha wiki moja ijayo.