Kesi kuhusu mauaji ya mwanamapinduzi wa Burkina Faso Thomas Sankara yaendelea Ouagadougou

  • Abdushakur Aboud

Thomas Sankara, Rais wa zamani wa Burkina Faso aliyeuliwa Oktoba 15, 1987

Kesi iliyokuwa inasubiriwa kuhusu mauaji ya mwana mapinduzi wa Burkina Faso na Afrika kwa ujumla Thomas Sankara imefunguliwa rasmi mjini Ouagadougou Jumatatu ambapo watu 14 akiwemo rais wa zamani wanatuhumiwa kwa mauaji hayo yaliyotokea mwaka 1987.

Itakuwa miaka 34 tangu kuuliwa kwa kiongozi huyo mashuhuri aliyetaka kuwakomboa wa Burkinabe na waafrika kutokana na "kasumba za ukoloni" lakini ndoto yake haikukamilika alipopinduliwa miaka minne baadae na marafiki zake wa karibu.

Tangu kuuliwa kwake Thomas Sankara, aliyefahamika kama Che Guevara wa Afrika, Waburkinabe daima wamekuwa wakimdhania rais aliyechukua nafasi yake rafiki yake mkuu Blaise Compaore, aliyetawala taifa hilo la ukanda wa Sahel kwa miaka 27, ndiye alihusika na mauaji hayo.

FILE - Rais wa zamani wa Burkina Faso Blaise Compaore katika kampeni yake ya uchaguzi.

Compaore alipinduliwa kutokana na mapinduzi ya wananchi 2014 na kukimbilia taifa jirani la Ivory Coast, lililompatia uraia.

Na katika juhudi za kutaka kufahamu ukweli na kuleta maridhiano nchini Burkina Faso, kiongozi aliyechaguliwa kwa njia ya kidemokrasia na aliyekuwa rafiki wa Sankara rais Roch Kabore anaunga mkono kesi hiyo.

Said Hilal mshauri wa Kabore na Campaore ameiambia Sauti ya Amerika kwamba kesi hiyo ni muhimu ili kuweza kufahamu ukweli na kufunga ukurasa mzito katika historia ya taifa hilo.

Hata hivyo wakili wa Compaore, Pierre-Olivier Sur alisema siku ya Ijumaa kwamba kiongozi huyo wa zamani hatashiriki kwenye kesi hiyo wakidai ni kesi ya kisiasa.

"Hawakutuarifu juu ya utaratibu huu, hatujapokea hati yoyote ya kusema tunatuhumiwa, wala kuruhusiwa waatalamu wetu, au kutoa ushahidi kabla ya kesi. Hakuna kilichofanyika na hivyo sisi tuna chukulia kuwa huu si utaratibu wa kisheria," amesema Sur.

Lakini Hilali anasema Compaore anakosa nafasi ya kihistoria kujitetea.

"Hii ingekuwa nafasi yake ya kihistoria kusema kile kilichotokea na kilichosababisha kuuliwa kwa Thomas Sankara," amesema Hilal.

Ingawa Sankara alitawala kwa muda mfupi sana lakini anachukuliwa kama shujaa wa taifa hata na wale ambao hawakuzaliwa alipokuwa madarakani. Watu waliotembelea makumbusho yake yaliyofungulwa mwaka 2017 wakizungumza na AFP wanasema wanataka ukwel ujulkane

"Matarajio yetu si makubwa, tunataka ukweli ujulikane, mwangaza umulike kuhusiana na kipindi hicho kibaya cha umwagikaji damu nchini kwetu, kwa hivyo tunataka kujua ukweli na haki itendeke," amesema Smockey, msanii mwanamuziki wa vuguvugu la Balai

Mariam Sankara, mjane wa Thomas Sankara rais wa zamani wa Burkina Faso

Mjane wa Sankara, Mariam amerudi nyumbani kuhudhuria kesi hiyo, na anasema amesikitishwa kwamba kiongozi huyo wa zamani ameamua kutohudhuria kesi hiyo. .

"Sio haki, kwa hakika sio haki kwa sababu hayupo hapa. Ilibidi awepo, ilibidi aonyeshe ushujaa wake kwa kufika hapa. Lakini kama unavyofahamu sio kila mtu ni shujaa wanakimbia kukabiliana na ukweli," amesema Mariam.

Naye mmoja kati ya washtakiwa wakuu jenerali Gilbert Diendere yuko mahakamini kusikiliza kesi dhidi yake. Na ikimalizika Said Hilali anasema kutakuwepo na mkutano mkuu wa kitaifa kuzungumzia suala la maridhiano na upatanishi. Na viongozi wa Burkina faso wanataka kuonyesha mfano mkubwa kwa nchi za Afrika kwamba haki inabidi itendeke na kuwepo maridhianio kuweza kupatikana maendeleo ya dhati.

Ingawa Compaore hatakuwepo wachambuzi na Waburkinabe wanamatarajio kwamba ukweli utaweza kujulikana.

Your browser doesn’t support HTML5

Kesi ya mauaji ya Thomas Sankara yaanza kusikilizwa