Jopo la majaji saba lilianza kusikiliza kesi hiyo leo asubuhi, na itaendelea kwa siku tano na hatimaye litaamua iwapo nchi hiyo itaitisha kura ya maoni ya kuifanyia Katiba marekebisho.
Viongozi wanaounga mkono BBI, wakiwa ni pamoja na Rais Uhuru Kenyatta, na kiongozi wa upinzani, Raila Odinga, wanatumai kuwa mahakama hiyo ya rufaa itasitisha utekelezaji wa uamuzi huo wa mahakama kuu.
Washirika hao wawili wa mpango wa maridhiano maarufu kama 'Handshake,' wamekuwa wakipigia upatu mchakato huo, wakisisitiza kuwa ni njia ya kuunganisha nchi, na kuimarisha mstakabali wa amani nchini humo. Mahakama kuu, ilitoa maamuzi kwamba mchakato huo ulikiuka katiba.
Wawili hao wanawakilishwa na mawakili sita ambao waliwasilisha hoja 31 za kupinga uamuzi wa mahakama kuu.
Mwanasheria mkuu wa Kenya pamoja na tume ya uchaguzi na mipaka, IEBC, pia wamejumuishwa kwenye rufaa hiyo.
Jopo hilo la mahakama ya rufaa linaongozwa na jaji Daniel Musinga.