Washambuliaji hao walimuua binti wa waziri huyo na dereva wake, msemaji wa jeshi na vyombo vya habari wamesema.
Waziri huyo ambaye ni kamanda wa zamani wa jeshi, alijeruhiwa.
Kituo cha Televisheni cha Uganda, NBS, kiliripoti kwamba washambuliaji wanne waliokua kwenye pikipiki walifyatua risasi, kwenye gari lililokuwa linambeba Jenerali Katumba Wamala. Shambulio hilo lilitokea katika kitongoji cha Kiasasi mjini Kampala.
“Kumefanyika shambulio la risasi lililomlenga yeye, amejeruhiwa na amepelekwa hospitali. Dereva wake aliuwawa,” msemaji wa jeshi Brigedia Flavia Byekwaso ameliambia shirika la habari la Reuters.
Mbunge Chris Baryomunsi amethibitishwa kwamba binti wa waziri Wamala, ambaye alikua naye ndani ya gari aliuwawa.
Miaka ya karibuni, kumekuwa na visa kadhaa vya mauaji, ambayo hayajafanyiwa uchunguzi wa kutosha, pamoja na vifo vya kushangaza ,vya maafisa mashuhuri katika nchi hiyo ya Afrika mashariki, ambayo yamechochea uvumi, juu ya wahusika na nia yao.
Miongoni mwa waliouwawa, ni mbunge, afisa wa polisi wa ngazi ya juu , muendesha mashtaka mkuu wa nchi, viongozi wa kiislamu na wengine. Karibu mauaji yote hayo yalitekelezwa na watu waliokua kwenye pikipiki.
-Imetayarishwa na Patrick Nduwimana